Welcome To Our Official Website

ASKARI POLISI WANNE WAFUKUZWA KAZI SHINYANGA

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Ernest Mangu

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limewafukuza kazi askari polisi wake wanne wakiwemo watatu wa kikosi cha usalama barabarani ambao wamefukuzwa kwa kosa la kupokea rushwa na kwenye magari barabarani na askari mwingine kwa kosa la utoro jeshini baada ya kujipa likizo mwenyewe.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa vyombo vya habari iliyotolewa Juni 16 ,2014  na kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga kamishina msaidizi wa polisi Kihenya Kihenya.

Kamanda Kihenya amesema kwa mujibu wa mamlaka aliyokasimiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IJP amewafukuza kazi askari polisi hao kwa fedheha kuanzia Juni 11,2014 kwa kosa la kufanya kitendo kibaya kinyume na mwenendo mwema wa jeshi la polisi cha kupokea rushwa wakiwa kazini tarehe 30,Machi,2014 majira ya mchana.

Kamanda Kihenya amewataja askari wa kikosi cha usalama barabarani waliofukuzwa kazi kuwa ni EX.F.899 koplo Jonathan James Bujiku,EX.WP.5198 Pc Joyce Malima Paul na EX.F 9839 pc Sohela Mabeho Kisinza.

Amesema askari hao walipokea rushwa ambayo thamani yake haikufahamika kutoka kwa kondakta,wahusika wa magari tofauti wakiwa kazini katika barabara kuu ya Shinyanga –Tinde eneo la Nhelegani katika manispaa ya Shinyanga.

Jeshi hilo la polisi pia limemfukuza kazi kuanzia Juni 12,2014 askari polisi EX.G.3829 pc Prosper Kayaya wa kazi za kawaida kwa kosa la utoro jeshini ambapo askari huyo alijipa likizo.


Kamanda Kihenya amekemea vitendo hivyo kwani ni kinyume cha mwenendo mwema wa jeshi la polisi huku akiwataka askari wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga kufanya kazi kwa uwazi,uaminifu na uadilifu mkubwa.

0 comments:

Post a Comment