Waandishi wa habari wakifuatilia kilichokuwa kinazungumzwa na viongozi wa Chama cha Baiskeli nchini (CHABATA) |
Waandishi wa habari wakiwa eneo la tukio |
Kamati ya tendaji ya chama cha Baiskeli taifa (CHABATA) imewasimamisha wajumbe wake wawili kutokana na utovu wa nidhamu waliouonesha ndani ya chama kama vile kusambaza taarifa za uongo katika vyombo vya habari ikiwemo kudai kuwa viongozi wa ngazi ya juu wa CHABATA wametafuna shilingi milioni 26 za mdhamini ambaye hata hivyo wajumbe waliosimamisha wamekuwa hawataji ni wadhamini gani.
Akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo tendaji ya Chabata taifa na waandishi wa habari mjini Shinyanga mwenyekiti wa chama cha Baiskeli nchini Godfrey Jax Mhagama amesema maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha kamati tendaji ya CHABATA iliyokaaa Juni 15,mwaka huu mjini Shinyanga.
Mhagama amesema miongoni mwa mambo yaliyoazimiwa katika kikao hicho ni kwasimamisha viongozi wawili ambao ni Lucas Bupilipili aliyekuwa katibu mkuu wa CHABATA mkoa wa Mwanza na Moses Andrew aliyekuwa kiongozi katika moja ya klabu ya baiskeli mkoani Arusha.
Amesema viongozi hao kuanzia sasa hawataruhusiwa kujishirikisha michezo ya baiskeli na kuzungumzia chochote kuhusu michezo ya mpaka pale utakapofanyika mkutano mkuu wa CHABATA ambao utatoa maamuzi kuhusu kusimamishwa kwa wajumbe hao.
Katika hatua nyingine Mhagama amesema kikao hicho cha mwisho katika nusu ya mwaka kilifanya mabadiliko ya katiba ya chama ambapo wameongeza kamati ya uongozi na sasa chama cha Baiskeli Zanzibar (CHABAZA) kimeingizwa katika chama cha Baiskeli Tanzania(CHABATA) na tayari walishafanya mazungumzo na CHABAZA kuhusu maamuzi hayo.
Mhagama amesema kikao hicho cha kamati tendaji kimemteua rasmi Kamanda Suleiman Kova kuwa mlezi wa chama huku wakili Magusu Mugoka akiteuliwa kuwa mwanasheria na Charles Kuziganika kuwa mhasibu wa CHABATA.
Aidha kikao hicho pia kimeteua wajumbe wawili wa baraza la wadhamini ambao ni mzee Shaaban Masamaki Bwire na mzee Leonard Derefa aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini mkoa wa Shinyanga.
Naye katibu mkuu wa CHABATA John Machemba ametumia fursa hiyo kuwaasa wajumbe wa chama hicho kufuata taratibu zinazotakiwa katika chama na kwamba hivi sasa chama kimejipanga vizuri kama taasisi kufanikisha malengo yao katika kuhakikisha kuwa CHABATA inafanikiwa hadi ngazi ya kimataifa.
Machemba amesema pamoja na kuwepo kwa tuhuma nyingi dhidi ya chama hicho mambo mengi zaidi watayawasilisha katika mkutano mkuu wa chama ambao watautumia kuwaeleza wapenzi wa baiskeli na watanzania kwa ujumla kuhusu mambo yanayoendelea katika chama na mchezo wa baskeli kwa ujumla
Na Kadama Malunde-Shinyanga
0 comments:
Post a Comment